Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSMIL yalaani mauaji ya wanaharakati Libya

UNSMIL yalaani mauaji ya wanaharakati Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umelaani mauaji ya mwanaharakati Entissar Al-Hasaeri yaliyotekelezwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Triopoli.Taarifa ya ujumbe huo inasema miili ya Al-Hasaeri na mwanamke mwingine Amal Al-Mizdawi, ilipatikana katika gari la wahanga hao mtaani mjini Tripoli siku ya Jumatatu Februari 23 mwaka huu.Hii ni kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na vikundi vya haki za binadamu nchini Libya. Taarifa zinasema wanaharakati hao walipigwa risasi vichwani.

UNSMIL umetaka mamlaka za nchini humo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji hayo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika.

Wanaharakati wa haki za binadamu, wanawake, na wale wa siasa pamoja na wanahabari wamekuwa wakiuwawa, kutekwa nyara na kutishwa.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umetaka mamlaka za Libya kuhakikisha makundi hayo yanalindwa pamoja na kuhakikisha utulivu nchini humo.