Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa Paraguay kwa UM wapongezwa

Mchango wa Paraguay kwa UM wapongezwa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Rais Horacio Cartes wa Paraguay mjini Asuncion ambapo ameshukuru nchi hiyo kwa mchango wake kwa Umoja wa Mataifa hususan ulinzi wa amani huko Haiti.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Ban akipongeza pia maendeleo ya Paraguay katika kufanikisha malengo ya milenia hasa katika lengo la kutokomeza umaskini.

Katika ziara hiyo ya kwanza kabisa kufanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ndani ya miaka 56, Ban amekaribisha jitihada za nchi hiyo iliyoko Amerika ya Kusini kwa kukabiliana na uzalishaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya.

Ameihamasisha Paraguay ishiriki pia katika maandalizi ya kikao maalum cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu tatizo la madawa ya kulevya duniani kitakachofanyika mwakani.

Bwana Ban ametumia pia fursa hiyo ya mazungumzo kupongeza Paraguay kwa kuchaguliwa kuwa mwanachama wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa akielezea imani yake kuwa itasaidia  harakati za nchi hiyo kushughulikia masuala ya haki ya ardhi kwa watu wa jamii za asili hasa pale kunapoanzishwa miradi ya maendeleo.

Katibu Mkuu ameitaka pia Paraguay kubadilishana na nchi nyingine uzoefu wake wa kuendeleza nishati mbadala.