Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzuiaji uhalifu na uzingatiaji wa haki vyaangaziwa Baraza Kuu

Uzuiaji uhalifu na uzingatiaji wa haki vyaangaziwa Baraza Kuu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa ngazi ya juu kuhusu jinsi ya kujumuisha suala la uzuiaji uhalifu na uzingatiaji wa haki kwenye ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Hoja ya msingi katika mjadala huo ni jinsi ya kushughuikia changamoto za kijamii na kiuchumi na kuendeleza maendeleo endelevu kwa kuzuia uhalifu na kuimarisha mifumo ya kushughulikia uhalifu huku viwango na maadili yakizingatiwa.

Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa akihutubia washiriki amesema kila uchao uhalifu unakwamisha maendeleo kwa kuwa..

(Sauti ya Kutesa)

“Kadri watu kila mahali wanapohaha kutumia vyema fursa za kiuchumi na kijamii kwa familia zao na kuinua kiwango cha maisha yao, tunafahamu kuwa ulinzi dhidi ya uhalifu na ghasia ni moja ya vigezo vya msingi vya kupata maisha yenye utu na tija.”

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson pamoja na mambo mengine akataja jambo linalopaswa kutiliwa maanani ni kuibuka kwa uhusiano kati ya uhalifu wa kupangwa na ugaidi akisema..

(Sauti ya Eliasson)

“Pande zote sasa kwa nia njema zinapaswa kuungana iwe za kimataifa na kitaifa ili kukabiliana na uovu huu. Nchi zote zinahitaji mifumo bora ya kuzuia na kuchunguza uhalifu.”