Myanmar irejee kwenye mkondo wa haki za binadamu- Zeid

25 Februari 2015

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, ameonya leo kwamba huenda Myanmar inakwenda mrama, na inapaswa kurejea kwenye mkondo sahihi haraka mwaka huu ambao ni muhimu kwa mpito wa demokrasia na maridhiano ya muda mrefu.

Kamishna Zeid amesema jamii ya kimataifa imeona mabadiliko Myanmar kama hadithi ya kutia moyo na matumaini, lakini matukio ya hivi karibuni kuhusu haki za binadamu za makundi ya walio wachache, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kufanya maandamano ya amani sasa yanafanya mabadiliko hayo kuhojiwa, huku vikitishia kusambaratisha ufanisi uliopatikana.

Akitoa mifano ya visa vya hivi karibuni, vikiwemo vile cha watu 14 wa jamii ya Michaungkan kufungwa kwa kufanya maandamano kuhusu jeshi kunyakuwa mashamba yao na kufungwa kwa wanahabari 10, amesema nafasi iliyokuwa imefunguliwa ya uhuru wa kujieleza na kufanya maandamano ya amani imebanwa tena kwa kutumia sheria kwa njia za kukandamiza.

Kamishna Zeid amesisitiza kuwa kuhakikisha kuna nafasi ya demokrasia kutakuwa muhimu kwa kura ijayo ya maoni kuhusu katiba na uchaguzi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud