Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO kumuenzi Profesa Mazrui kupitia chapisho alilohariri

UNESCO kumuenzi Profesa Mazrui kupitia chapisho alilohariri

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika tukio maalum la kumbukizi ya mchango wa mwanamajumui na nguli wa fasihi barani Afrika Profesa Ali Mazrui aliyeaga dunia mwezi Oktoba mwaka jana.

Shughuli hiyo iliandaliwa na ujumbe wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na Utamaduni, UNESCO ambapo shirika hilo limesema litamuenzi msomi huyo kwa kujumuisha barani humo mradi wa Historia ya Afrika.

Mkuu wa ofisi ya UNESCO jijini New York, Dkt. Moufida Goucha alisema hayo katika hotuba yake akisema hayati Profesa Mazrui alishiriki katika kuandika na hata kuhariri juzuu ya Nane ya mradi huo kama anavyofafanua Lily Valtchanova wa UNESCO.

(Sauti ya Lily)

“Hivi sasa tuna mpango wa kushirikiana na wizara za elimu za Afrika ili ziweze kujumuisha mradi wa Historia ya Afrika kwenye mitaala yao ya elimu.”

Kwa mujibu wa Bi. Valtchanova, mradi huo umesaidia kubadili mtazamo wa dunia kwa Afrika.

(Sauti ya Lily)

“Watu wenye asili ya Afrika wanaoishi Afrika au watu wenye asili ya Afrika wanaoishi ughaibuni wote wanapaswa kujivunia ustaarabu na asili ya utamaduni wa Afrika.”