Cote d’Ivoire ni mfano wa kuiga katika kukomesha ukosefu wa utaifa: UNHCR

24 Februari 2015

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa kushirikiana na taasisi ya uchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, wanaendesha mkutano wa mawaziri kuhusu ukomeshwaji wa kutokuwa na utaifa.

Mkutano huu wa kipekee barani Afrika utafanyika mjini Abidjan nchini Côte d’Ivoire Februari 25 na unalenga kutafuta suluhisho la kikanda katika kuzuia, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa suala la raia kutokuwa na utaifa Afrika Magharibi.

Akizungumza na Rais Alassane Ouattara wa Cote d’Ivoire siku moja kabla ya mkutano huo, Kamishna Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres ameipongeza serikali ya Cote d’Ivoire kwa jitihada zake katika kurejesha wakimbizi nchini na kutatua swala la raia wasiokuwa na utaifa.

“ Mabadiliko muhimu sana ya kisheria na kiutendaji yametekelezwa nchini Cote d’Ivoire ili kutatua shida ya ukosefu wa utaifa nchini humo. Ni mfano wa ufanisi unaopaswa kuigwa kote duniani. Na mfano huo ni muhimu sana kwa sisi.”

Kwa mujibu wa UNHCR zaidi ya watu 750,000 hawana utaifa au wako katika hatari ya kukosa utaifa Afrika Magharibi.

Sababu za ukosefu wa utaifa zilizotajwa na UNHCR ni pamoja na kutokuwa na mpango wa usajili wa raia na ukosefu wa usajili wa watoto wanapozaliwa.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la wakimbizi linakadiria kuwa takribani watu milioni 10 kote duniani hawana utaifa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter