Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kukwamua raia wa Ukraine wazinduliwa

Mpango wa kukwamua raia wa Ukraine wazinduliwa

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamezindua leo mpango wa usaidizi kwa raia wa Ukraine kwa mwaka 2015. Mpango huo wa usaidizi unawalenga watu milioni 3.2 kati ya milioni 5 wanaohitaji msaada wa kibinadamu nchini humo. Jumuiya ya kimataifa imeombwa kutoa kiasi cha zaidi ya dola milioni 300 ili kuokoa maisha ya raia, ikiwa ni pamoja na ugawaji wa chakula, vifaa vya majumbani , huduma za afya, msaada wa kisaikolojia, malazi, mavazi ya kujikinga na baridi na elimu ya msingi.

Kwa mujibu wa mratibu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadmau ya Umoja wa Mataifa OCHA, nchini Ukraine Neal Walker, tangu mwezi Januari mahitaji ya raia yameongezeka huku maisha ya waliotatizwa na mgogoro yakizidi kuwa hatarini .

Amesema uwezo wa nchi hiyo kuwahudumia wahanga wa machafuko ni mdogo huku ikikadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja hawana makazi nchi nzima na wengine milioni mbili wakigombea maeneo ya kujihifadhi.

Walker amesema msaada wa jumuiya ya kimatifa ni muhimu ili kukwamua jamii hizo.