Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahanga wa mafuriko Malawi wasaidiwa

Wahanga wa mafuriko Malawi wasaidiwa

Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM na Shirika la Mpango wa Chakula duniani WFP yanasambaza msaada kwa ajili ya watu waliolazimika kuhama makwao nchini Malawi, kufuatia mafuriko ya mwezi Januari.

Kwa mujibu wa IOM, takriban watu 230,000 wamepoteza makazi yao, na mahitaji ya wakimbizi hao yanazidi uwezo wa utoaji msaada uliopo nchini humo kwa sasa.

Msaada wa IOM unalenga hasa kuimarisha uongozi katika kambi za wakimbizi, na ufuatiliaji wa mahitaji ya kibinadamu.

Kwa upande wake WFP imetangaza kuwafikishia chakula watu zaidi ya 288,000, huku mvua zikiendelea kunyesha.

Zaidi ya tani 200 zimesambazwa kwa njia ya ndege katika maeneo yasiyofikishwa tena kwa njia ya barabara kutokana na mafuriko.

Aidha WFP imesema takriban watu 700,000 wanahitaji msaada wa chakula nchini humo, na shirika hilo limetoa ombi la ufadhili wa dola milioni 3.3 kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu.