Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji haramu wa binadamu kuangaziwa Malaysia

Usafirishaji haramu wa binadamu kuangaziwa Malaysia

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wanaosafirishwa kinyume cha sheria Maria Grazia Giammarinaro ameanza ziara ya siku sita nchini Malaysia ili kujionea hali halisi ya vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu nchini huko akijikita katika athari za vitendo hivyo kwa wanawake,wanaume, wasichana na watoto.

Akiwa nchini humo kufuatia ziara ya serikali ya Malaysia, anatarajia kukutana nao na kusikiliza madhila wanayokumbana nayo akisema serikali ina wajibu wa kusikiliza kilio cha watu hao.

Umoja wa Mataifa unasema wanawake, wasichana na watoto kutoka Thailand, Cambodia, Myanmar na Vietnam wanazidi kusafirishwa kwenda Malaysia na kutumikishwa kwenye ukahaba.

Kwa mantiki hiyo akiwa nchini humo Bi. Giammarinaro atahamasisha mikakati ya kukabiliana na utumikishwaji kwenye ajira na utetezi wa haki za binadamu atakapokutana na maafisa wa serikali na wa mashirika ya kiraia.

Ripoti ya mtaalamu huyo ataiwasilisha kwenye Baraza la haki za binadamu mwezi Juni mwakani.