Ban alaani shambulio Mogadishu na Qubbah

20 Februari 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la kigaidi kwenye hoteli moja kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Shambulio hilo limesababisha vifo ambapo waliojeruhiwa ni pamoja na viongozi wa serikali na wabunge.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yake amesema tayari Ban amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Somalia.Hassan Sheikh Mohamud, ambapo ametuma rambirambi kwa serikali na familia za waliofiwa pamoja na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.

Katibu mkuu pia ametoa shukrani kwa vikosi vya Somalia kwa jinsi walivyoshughulikia tukio hilo na kuweka udhibiti huku akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusimama kidete kusaidia wananchi wa Somalia na serikali yao ili kujenga amani na ustawi.

Amesisitiza kuwa shambulio hilo kigaidi kamwe halitakatisha tamaa ari ya wananchi wa Somalia wala azma ya Umoja wa Mataifa ya kutaka kusonga mbele.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu amelaani vikali mashambulio kwenye mji wa mashariki mwa Libya, Qubbah, ambayo yameripotiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Ametuma rambirambi zake kwa wananchi wa Libya akisema vitendo hivyo vya kigaidi vinakumbusha kuwa suluhu la kisiasa kwenye mzozo nchini humo linapaswa kupatikana haraka iwezekanavyo ili kurejesha amani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud