Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jengo la sheria ya kimataifa kuanza kujengwa mjini Arusha

Jengo la sheria ya kimataifa kuanza kujengwa mjini Arusha

Umoja wa Mataifa umesaini leo kandarasi na shirika la Jandu Plumbers Ltd., ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la mfumo wa mahakama za uhalifu wa kimataifa, MICT, mjini Arusha, Tanzania.

Mradi huo wa ujenzi unatazamiwa kuanza hivi karibuni, na kuendelea kwa kipindi cha miezi 12.

Mapema mwezi huu, hatua nyingine muhimu ilipigwa katika mradi huo, pale barabara ya kuenda kwa jengo hilo ilipoanza kujengwa, huku huduma za maji, umeme na intaneti zikitarajiwa kufikishwa hapo hivi karibuni.

Akizungumza mbele ya maafisa wa serikali ya Tanzania waliokusanyika kwenye eneo la ujenzi kushuhudia kuanza kwa kazi ya kujenga barabara, Msimamizi wa MICT, John Hocking, ameelezea shukrani zake kwa serikali ya Tanzania kwa kujikita katika kutimiza ahadi ya kukamilisha mradi huo katika muda mwafaka.

Amesema jengo hilo litakuwa siyo tu jengo lenye umaarufu mkubwa mjini Arusha, lakini pia kielelezo cha ulimwengu kujikita katika kuendeleza sheria kwenye ngazi ya kimataifa.