Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni yazinduliwa watoto waende shule Sudan Kusini:

Kampeni yazinduliwa watoto waende shule Sudan Kusini:

Takribani watoto 400,000 nchini Sudan Kusini ambao masomo yao yamekatishwa kutokana na mzozo unaoendelea nchini mwao watakuwa na fursa ya kwenda shuleni ndani ya mwaka mmoja ujao.

Mpango huo unawezekana kufuatia kampeni ya Rejea Masomoni iliyozinduliwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF huko Juba, Sudan Kusini na kuhudhuriwa na Rais Salva Kiir Mayardit.

Watoto katika majimbo yote 10 ya nchi hiyo watafikiwa na kampeni hiyo ikiwemo maeneo ambayo bado yana mapigano.

Mwakilishi wa UNICEF Sudan Kusini Jonathan Veitch amesema watashirikiana na wadau wao kufikia watoto wenye umri wa kati ya miaka mitatu hadi 18 kwenye maeneo hayo hatarishi kwa gharama ya dola 100 kwa kila mtoto.

Hata hivyo Veitch amesema wanahitaji nyongeza ya dharura ya dola Milioni 12 ili kuhakikisha wanapeleka vifaa vya msingi vya elimu kwenye shule zilizolengwa.

Takribani asilimia 70 ya shule 1,200 kwenye maeneo ya mzozo zimefungwa hali inayoongeza hofu kuwa kizazi cha sasa kitabakia mamuma kutokana na mapigano yanayoendelea.