Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaoshikiliwa kinyume cha sheria Syria waachiliwe huru: Zeid

Wanaoshikiliwa kinyume cha sheria Syria waachiliwe huru: Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameitaka serikali na vikundi vilivyojihami Syria kuachilia huru wale wote wanaoshikiliwa korokoroni kinyume cha taratibu.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu imemnukuu Kamishna Zeid akisema wengi wameshikiliwa kwa zaidi ya mwaka bila taratibu zozote za kimahakama na hiyo inatia shaka kutokana na kuenea kwa vitendo vya utesaji na udhalilishaji kwenye maeneo hayo.

Ametolea mfano wanaharakati watatu, Mazen Darwish, Hani Al-Zaitani na Hussein Ghrer, ambao wanashikiliwa kwa miaka mitatu sasa kwa tuhuma za ugaidi.

Amesema mwezi  uliopita kesi yao iliahirishwa kwa mara ya sita na hakuna tarehe mpya imepangwa ili iweze kusikilizwa.

Kamishna Zeid amesema katika visa vingi watu hushikiliwa kwa wiki au miezi kadhaa bila kufahamika waliko na hata kuwa na mawasiliano.

Ameitaka serikali ya Syria kuwaachia huru mara moja wale wote ambao wanashikiliwa kwa kisa tu cha kujieleza au kutoa maoni na sambamba na hiyo wale wenye kesi mchakato wa sheria ufuatwe.