Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na udhibiti wa bidhaa zinazoleta utipwatipwa kwa watoto

WHO na udhibiti wa bidhaa zinazoleta utipwatipwa kwa watoto

Shirika la afya duniani, WHO kanda ya Ulaya imeandaa muundo wa kuwezesha nchi za ukanda huo kukabiliana na matangazo yanayohamasisha vyakula na vinywaji vyenye kiwango kikubwa cha sukari, chumvi na mafuta. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

WHO inasema kwa kuzingatia ongezeko la utipwatipwa miongoni mwa watoto barani Ulaya na kwingineko, hakuna jambo lolote linalohalalisha matangazo ya vyakula visivyo na nyongeza yoyote ya lishe kwa watoto.

Dkt. Gauden Galea wa WHO kanda ya Ulaya amesema imekuwa vigumu kubaini vyakula ambavyo matangazo yake yanapaswa kudhibitiwa kwenye televisheni, mabango, intaneti na hata maeneo mengine, lakini sasa mbinu mpya imepatikana.

Mbinu hiyo ni sera inayotoa mwongozo wa virutubisho kwa watoto ambapo nchi zinaweza kuutumia kulingana na eneo lao ili kubaini aina za vyakula ambavyo matangazo yake yanafaa kwa watoto na hatimaye kuboresha afya zao.