Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata uchaguzi DRC, MONUSCO kuhamasisha jamii ya kimataifa

Ukata uchaguzi DRC, MONUSCO kuhamasisha jamii ya kimataifa

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO utasaidia kuhamasisha jamii ya kimataifa ili kuziba pengo la fedha zinazohitajika kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015 na 2016 nchini humo, amesema leo msemaji wake Charles Bambara.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, msemaji huyo wa MONUSCO amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa yanajituma ili kuhakikisha kuna ufadhili wa kutosha kwa ajili ya uchaguzi huo utakaogharimu zaidi ya dola Bilioni Moja.

Ameongeza kwamba mkuu wa MONUSCO Martin Kobler anakutana mara kwa mara na mabalozi waliopo nchini DRC ili kuwahamasisha kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya uchaguzi.

Wiki iliyopita Kamisheni ya Kitaifa ya Uchaguzi CENI ilitangaza ratiba ya uchaguzi ambapo uchaguzi wa rais na bunge utafanyika mwezi Novemba mwaka 2016, wakati uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Oktoba mwaka huu.