Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya Ebola vinapungua mara 10 zaidi kila wiki kuliko Septemba 2014- Nabarro

Visa vya Ebola vinapungua mara 10 zaidi kila wiki kuliko Septemba 2014- Nabarro

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ebola, David Nabarro, amesema leo kuwa visa vya Ebola vinapungua mara kumi zaidi kila wiki kuliko hali ilivyokuwa mwezi Septemba mwaka jana. Hata hivyo, Dkt Nabarro ameonya kuwa, kuzuia asilimia 10 ya mwisho ya maambukizi huenda kikawa ndicho kitendawili kigumu zaidi cha mapambano. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Dkt. Nabarro amesema hayo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo limekutana kusikiliza ripoti ya hivi karibuni zaidi kuhusu tatizo la Ebola Afrika Magharibi na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia dharura ya tatizo hilo.

Mjumbe huyo maalum wa Katibu Mkuu amesema kuwa hatua kubwa zimepigwa katika kupambana na Ebola, lakini akaonya kuwa juhudi za mapambano ni lazima ziendelee hadi asilimia 10 ya mwisho ya visa vya maambukizi vizuiliwe

“Hadi sehemu hiyo ihitimishwe, nchi zilizoathiriwa na ulimwengu hauwezi kutangaza ushindi. Mlipuko wa Ebola hautaisha hadi kisa cha mwisho kitambuliwe na kutibiwa. Mfumo wa Umoja wa Mataifa utaendelea kujikita kikamilifu katika mapambano hadi mlipuko huu kuisha na katika kipindi cha kujikwamua.”

Dkt. Nabarro amesema Umoja wa Mataifa na wadau watahitaji ufadhili wa ziada ili kutoa usaidizi kwa serikali za kitaifa zinapojitahidi kukomesha maambukizi.

Akihitimisha, ametoa mwelekeo wa siku zijazo

“Tunajua kuwa kutakuwa na milipuko ya homa ya kuvuja damu na magonjwa mengine siku zijazo. Wakati huu wote, mapambano yetu yanaangazia njia za kutumia mafunzo ili mataifa na kanda zinaweza kukabiliana haraka na ipasavyo na hatari siku zijazo.”

Naye Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema kuna dalili za kutia moyo, huku akitoa tahadhari

“Lakini kazi muhimu zaidi bado ipo mbele yetu, hadi idadi katika nchi zilizoathiriwa ifikie sifuri, na kuanza ujenzi tena na ukwamuaji. Ni lazima tuzisaidie kuwa na uhimili zaidi. Ebola isiruhusiwe kukita tena mizizi katika ukanda huo.”