Baada ya ukame Cabo Verde, FAO yaeleza msaada
Shirika la chakula na kilimo duniani FAO limesema litawapatia msaada wa mbegu za mazao, chakula cha mifugo na vifaa vya umwagiliaji maelfu ya wananchi wa Cabo Verde ambao maisha yao yamekumbwa na mwambo baada ya ukame wa mwaka jana kuathiri shughuli za kilimo na mifugo.
Makubaliano ya msaada huo wenye thamani ya dola Laki Tano yametiwa saini mjini Roma wakati mkutano kati ya Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva na Waziri Mkuu wa Cabo Verde José Maria Pereira Neves.
Bwana Neves amesema makubaliano hayo siyo tu yatawezesha kukabiliana na ukame wa sasa bali pia yataweka mazingira ya kujenga kilimo endelevu nchini mwake.
Msaada huo utawezesha pamoja na mambo mengine kaya 7,015 kupatiwa kikasha cha uzito wa kilo 17 zinazojumuisha mbegu za mahindi, maharagwe meupe.
Halikadhalika kaya 554 ambazo miundombinu yao ya umwagiliaji imeathirika kutokana na kupungua kwa mvua zitapatiwa mbegu za nyanya, kabichi na vitunguu kama sehemu ya usaidizi wa dharura.