Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wa raia Sudan Kusini ni jukumu la msingi la UNMISS

Usalama wa raia Sudan Kusini ni jukumu la msingi la UNMISS

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Ellen Margrethe Loj, ametembelea mji wa Bor, nchini Sudan Kusini, ili kuelewa zaidi utekelezaji wa majukumu ya ujumbe huo hadi maeneo ya vijijini.

Wakati wa ziara hiyo ameshiriki sherehe za utoaji nishani ya ulinzi wa amani kwa walinda amani kutoka Ethiopia kwenye eneo hilo ambapo ameipongeza Ethiopia kwa mchango wake mkubwa katika operesheni za kulinda amani kwenye ukanda wa Afrika.

Kwa mujibu wa UNMISS, Ethiopia ni nchi ya kwanza kwenye ukanda wa Afrika kwa kuchangia wanajeshi wa kulinda amani. Nchini Sudan Kusini pekee, idadi ya walinda amani wa Ethiopia ni 1,200.

Halikadhalika ametembelea pia hospitali ya kijeshi ya wasrilanka ambayo imeshatibu watu 1.360 tangu kuundwa kwake mwezi Juni, mwaka uliopita.

Aidha mkuu wa UNMISS amesema ni jukumu la msingi wa ujumbe huo kulinda raia, wakiwa ndani au nje ya kambi za UNMISS, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwepo kwa usalama katika jamii.

Watu zaidi ya 100,000 wametafuta hifadhi katika kambi za UNMISS baada ya kuibuka kwa mzozo wa kisiasa nchini humo, Disemba, mwaka 2013.