Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la Baraza la Usalama launga mkono mapendekezo ya amani Ukraine

Azimio la Baraza la Usalama launga mkono mapendekezo ya amani Ukraine

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limepitisha kwa kauli moja azimio la kuunga mkono fungu la mapendekezo ya njia za kutekeleza makubaliano ya Minsk, Ukraine, ambayo yalilenga kupatia mzozo wa Ukraine suluhu la kisiasa. Fungu hilo la mapendekezo liliafikiwa mnamo Februari 12, 2015.

Baraza la Usalama pia limekaribisha tangazo la Marais wa Urusi, Ukraine, Ufaransa na Waziri Mkuu wa Ujerumani la kuunga mkono fungu hilo la mapendekezo, na pia kukaribisha ahadi zao za kutekeleza makubaliano ya Minsk.

Wakati huo huo, Baraza hilo limetoa taarifa iliyoelezea masikitiko yake kuhusu kuendelea kwa mapigano karibu na ndani ya Debaltseve, Ukraine, ambayo yamesababisha vifo vya raia wengi.

Taarifa hiyo imesema, licha ya tangazo la kusitisha mapigano mnamo Februari 15, machafuko yameendelea siku chache zilizopita katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine.

Wanachama wa Baraza hilo wamezitaka pande zote zisitishe uhasama mara moja, na kutimiza ahadi zilizowekwa katika makubaliano ya Minsk, na pia kujali utu wa watu wanaozuiliwa.