Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS yatangaza mipango ya 2015 kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini

UNMAS yatangaza mipango ya 2015 kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na huduma za kung’oa mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS limechapisha ratiba ya miradi itakayofanyika mwaka huu wa 2015, ambayo inalenga kulinganisha mahitaji ya nchi zilizoathiriwa na uwezo wa ufadhili. Jumla ya dola milioni 296 za Kimarekani zinahitajika kufadhili miradi hiyo, inagwa ni asilimia 20 tu, au dola milioni 57 ndizo zilizotolewa kufikia sasa.

Nchi yenye mahitaji makubwa zaidi ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini ni Afghanistan, ikifuatiwa na Cambodia.

Ratiba hiyo imetolewa wakati Mkurugenzi wa Shirika la UNMAS Agnès Marcaillou, akitangaza kuwa wakurugenzi wa kitaifa wa huduma za kuchimba mabomu ya ardhini wanakutana wiki hii mjini Geneva katika mkutano wa 18 kimataifa wenye kauli mbiu: “Zaidi ya Mabomu ya Ardhini: Kubadilika kwa Huduma za kukabiliana na Mabomu ya Kutegwa ardhini”

Bi Marcaillou amekumbusha kuwa mbali na mabomu ya kutegwa ardhini, huduma za shirika hilo zinamulika pia  zana za vita zinazolipuka, zile ambazo hazijalipuka, na zile zinazoundwa kienyeji, na ambazo huwaua wahudumu wa kibinadamu, walinda amani, wanahabari na wengineo.