Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuna mpango wa kupunguza usaidizi Yemen: WFP

Hatuna mpango wa kupunguza usaidizi Yemen: WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema licha ya changamoto za kiusalama nchini Yemen, operesheni zake hazijakumbwa na madhara yoyote na usambazaji wa misaada muhimu unaendelea kama kawaida.

Msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema kwa siku kadhaa mji mkuu Sana’a umekuwa tulivu huku maduka na masoko yakiwa wazi lakini hali bado ni ya wasiwasi mkubwa.

Hata hivyo amesisitiza kuwa licha ya hali hiyo hakuna mpango wa kupunguza operesheni za WFP nchini humo kwani wameweza kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa mamlaka waliyopatiwa.

Mwezi huu wa Februari WFP imepanga kufikishia msaada wa chakula watu Milioni Moja wakiwemo waliopoteza makazi nchini Yemen.

Hata hivyo Byrs amesema wanahtiaji kuchangisha dola Milioni 146 ili kufanikisha operesheni yake hiyo ya usaidizi kwa miezi 12 ijayo.