Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD yajikita zaidi katika maendeleo vijijini

IFAD yajikita zaidi katika maendeleo vijijini

Mabadiliko vijijini na umuhimu wake katika maendeleo endelevu ndiyo ajenda kuu katika kikao cha 38 cha baraza la uongozi la mfuko wa kimataifa wa kilimo na maendeleo (IFAD) unaofanyika mjini Rome Italia.

Kwa mujibu wa IFAD, wakati asilimia 70 ya idadi ya watu duniani itakuwa ikiishi mijini ifikapo mwaka 2050, wakulima wadogowadogo wana mchango mkubwa katika  maendeleo endelevu na usalama wa chakula.

Shirika hilo katika taarifa yake kuhusu kikao hicho cha siku mbili linasema maeneo yote ya mijini na vjijini hayawezi kufanikiwa bila kutegemeana na kuongeza kuwa msisitizo katika kikao ni maendeleo.

 IFAD inasema kuwa malengo ya  maendeleo endelevu (SDGs)ni fursa ya kufanikisha maendeleo ambayo ni jumuishi, na yanayowalenga watu. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa robo tatu ya maskini na wanaokabiliwa na njaa duniani wanaishi vijijini katika nchi zinazoendela.