Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lataka waasi wa Hoathi kuachia utawala wa serikali ya Yemen

Baraza la usalama lataka waasi wa Hoathi kuachia utawala wa serikali ya Yemen

 Baraza la usalama limetaka kundi la waasi wa Houthi nchini Yemen kuachia utawala wa serikali ya Yemen.

Hayo ni maamuzi kufuatia kikao cha baraza hilo kilichokutana leo Jumapili, ambapo baraza hilo limewataka waasi hao kuachia utawala wao katika taasisi nchini Yemen.

Wajumbe 15 wa baraza la usalama bila kupingwa  walipitisha azimio ambalo limepinga vikali hatua zaa waasi wa Houthi kulifuta bunge na kushika hatamu ya serikali ya Yemen na taasisi zake.

Kumekuwa na sintofahamu nchini humo kufuatia maandamano ya raia yalioanza mwaka 2011.

Baraza la usalama limetaka pande husika nchini Yemen kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na mashauriano huku wakitupilia mbali machafuko ili kufanikisha malengo ya kisiasa

.Limetaka waasi wa Houthi haraka na bila masharti kutoa vikosi vyao katika taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na mji mkuu Sana'a.

Kadhalika baraza la usalama limetaka kundi hilo kushiriki haraka katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa bila masharti yoyote.

Limetaka pande zote nchini Yemen kukubaliana na kutangaza hadharani tarehe za kukamilisha mashauriano ya katiba, na kuwa na rasimu ya katiba kisha kuendesha uchaguzi.

Mark Lyall Gant ni mwakilshi wa kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa

"Leo tumeweka wazi kuwa wale wanaotumia machafuko na vitisho kujaribu kutawala kimabavu mustakabali wa Yemen, wanazorotesha usalama wa raia wa Yemen na kudidimiza hatua za kisiasa zilizopigwa tangu mwaka 2011.Waasi wa Houthi lazima wawajibike kwa vitendo vyao na kuacha kutumia machafuko na kutumia nguvu kama nyenzo za kisiasa. Lazima wahakikishe kuachiwa haraka na salama kwa Rais Hadi, Waziri Mkuu Bahah na mawaziri kutoka katika nyumba wanazoshikiliwa"

Baraza la usalama pia limesema liko tayari kuchukua hatua za ziada ikiwa hakuna utkekelezaji kutoka kwa upande wowote nchini Yemen kuhusu azimio hili.