Yemen: Licha ya vurugu, UNICEF yaendelea kutoa usaidizi wa kibinadamu

13 Februari 2015

Licha ya mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Yemen, na kuzorota kwa hali ya usalama, bado mashirika ya kibinadamu yanaendelea kusambaza misaada nchini kote. Hii ni kwa mujibu wa Julien Harneis, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, ambaye amezungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva.

Harneis amesema UNICEF inaendelea na jitihada zake katika kupambana na utapiamlo na kuimarisha uandikishaji watoto shuleni nchi humo, na kwa kipindi cha miaka michache, uandikishaji huo umefanikiwa kufikia asilimia 70.

Hata hivyo, mwakilishi huyo ameelezea wasiwasi wa UNICEF wa kuona watoto wengi zaidi wakiathiriwa na utapiamlo na kuacha shule kutokana na kuzorota zaidi kwa hali ya uchumi na kusitishwa kwa huduma za serikali, mzozo wa kisiasa ukiendelea.

“ Tayari zaidi ya asilimia 60 ya raia wa Yemen wanaishi kwenye hali ya umaskini. Na hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya mzozo huo wa kisiasa. Tayari Yemen iko kwenye wakati mgumu, ni muhimu sana UNICEF na mashirika mengine yabaki nchini humo kwa ajili ya kusaidia watoto wa Yemen”

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto zaidi ya 900,000 wanaathirika na utapiamlo nchini humo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter