Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta imara ya usalama ni msingi wa amani endelevu: Eliasson

Sekta imara ya usalama ni msingi wa amani endelevu: Eliasson

Uboreshaji wa sekta ya usalama ni swala linalozingatiwa zaidi siku hizi katika Umoja wa Mataifa ambapo watalaam wa ulinzi wa amani na maendeleo wanasisitiza ni msingi wa kujenga amani endelevu. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katika mkutano uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu swala la Uboreshaji wa Sekta ya Usalama, Rais wa Baraza Kuu la Umoja huu amesema uboreshaji wa sekta hiyo ni hatua muhimu katika kujenga upya mamlaka za serikali za nchi zilizoathirika kwa vita au mizozo.

Kwa upande wake Jan Eliasson, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema uhalifu na ukosefu wa usalama ni kikwazo kikubwa sana katika maendeleo :

« Kwa sababu hiyo, inafaa kwamba serikali zizidi kuwekeza katika usalama, lakini, tulivyoelewa sisi sote, matumizi katika sekta ya usalama bila utawala bora na utawala wa sheria si lazima yasababishe utulivu wa hali ya juu kwa raia, nchi, ukanda, halikadhalika maendeleo.”

Amesisitiza kwamba uboreshaji wa sekta ya usalama unapaswa kwenda sambamba na utawala wa sheria, makubaliano ya kisiasa na kuheshimu haki za binadamu.