Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaiomba Ulaya kurejesha operesheni za kuokoa maisha Bahari ya Mediterenia

UNHCR yaiomba Ulaya kurejesha operesheni za kuokoa maisha Bahari ya Mediterenia

Kufuatia ajali za boti wiki hii kwenye bahari ya Mediterenia na vifo vya mamia ya wakimbizi na wahamiaji, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limetoa wito kwa Muungano wa Ulaya, EU, kubadili haraka mfumo wake wa kukabiliana na watu wanaovuka bahari ili kuhakikisha kuwa uokoaji wa maisha ndilo jambo la kipaumbele.

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Antonio Guterres amesema kuwa baada ya matukio ya wiki hii, ni dhahiri kuwa mfumo wa operesheni ya Ulaya wa Triton ni duni zaidi, kuliko ule wa zamani wa Italia uitwao Mare Nostrum, akiongeza kuwa operesheni kati mwa Bahari Mediterenia isiwe tu kuhusu udhibiti wa mipaka, bali iwe iangazie uokoaji wa maisha.

Guterres amesema uvukaji wa wahamiaji kwenye Bahari Medieterenia umekuwepo kwa miaka mingi, lakini mwaka 2014 ulishuhudia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofanya safari hiyo hatarishi, hali ambayo ilichangiwa na mizozo ya Syria, Pembe ya Afrika na maeneo ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Watu wapatao 218,000 walivuka Bahari Mediterenia, huku watu 3,500 wakipoteza uhai wao.

UNHCR imekuwa ikielezea masikitiko yake kufuatia kukomeshwa operesheni za Mare Nostrum, ambazo zilianzishwa na Italia kufuatia majanga kwenye kisiwa chake cha Lampedusa mnamo mwaka 2013, na ambazo ziliokoa maisha ya mamia ya wahamiaji.