Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubinafsishaji elimu ya msingi ni janga: Mtaalamu

Ubinafsishaji elimu ya msingi ni janga: Mtaalamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya elimu, Kishore Singh amezitaka serikali kutupilia mbali wazo la kubinafsisha sekta ya elimu ya msingi akisema kwa kufanya hivyo watoto kutoka familia maskini watapokonywa haki hiyo.Amesema hayo baada ya wataalamu wa elimu kutoka nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kukutana Rwanda wiki hii na kujadili pamoja na mambo mengine uwezekano wa kupunguza gharama za serikali kwenye elimu.

Bwana Singh amesema ana hofu kubwa kwamba baadhi ya serikali zinapigia chepuo ubinafsishaji wa elimu ya msingi akisema elimu siyo haki ya matajiri na wenye uwezo tu, bali ni haki aliyozaliwa nayo kila mtoto na hivyo utoaji elimu bila gharama ni wajibu wa msingi wa serikali.

Hivyo ametaka serikali kuliko wakati wowote ule kuongeza fursa za elimu ya msingi ya inayoratibiwa na serikali ili watoto wote hususan wale kutoka familia maskini waweze kunufaika.