Mazungumzo ya kisiasa Libya yaanza mjini Ghedames
Awamu nyingine ya mazungumzo ya kisiasa yanayoratibiwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, yameanza leo mjini Ghedames, Libya, huku wote walioalikwa kushiriki wakihudhuria mazungumzo hayo kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNSMIL, mazungumzo hayo yamefanyika kwa njia ya kujenga na mazingira mazuri, huku washiriki wakikubaliana kuendelea na mazungumzo siku chache zijazo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Libya na Mkuu wa UNSMIL, Bernardino Leon, amefanya mikutano mbali mbali na wawakilishi wa pande husika, akiwapa maelezo kuhusu mchakato huo wa kisiasa na ratiba yake na kuelezea kufurahiswa na moyo wa washiriki unaotia matumaini.
Mazungumzo ya siku ya kwanza yamemulika mada zilizokubaliwa katika ajenda, yakiwemo mapendekezo ya kuratibu kazi ya siku zijazo na kukubaliana kuhusu ratiba inayozingatia hamu ya pande husika kufikia suluhu la kisiasa haraka ili kuepusha kuzorota zaidi kwa hali ya usalama na kisiasa, pamoja na kumaliza migawanyo ya kitaasisi ambayo inatishia umoja wa taifa hilo.