29 wazama maji Lampedusa, UNHCR yazidi kupaza sauti
Kufuatia janga lingine la vifo vya watu 29 kwenye pwani ya Lampedusa siku ya Jumatatu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeendelea kusihi Umoja wa Ulaya kuimarisha huduma za uokozi kwenye eneo hilo.
UNHCR imesema inasikitishwa zaidi na jinsi watu hao walivyopoteza maisha kwani saba kati yao walifariki dunia wakiwa ndani ya chombo cha uokozi. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR Geneva.
(Sauti ya Adrian)
“Wakati tunapongeza wote waliohusika kwenye uokozi uliofanyika kwenye bahari kuu na hali mbaya ya hewa na kuwezesha kuokolewa kwa watu 106, tukio hili linatukumbusha kwa nini baada ya janga la Lampedusa Oktoba 2013 kulitakiwa kuwepo na mbinu thabiti zaidi za uokozi Mediteranian kwa kuzingatia kiwango cha watu wanaovuka eneo hili.”
Mwaka 2014 takribani watu 218,000 walitumia bahari ya Mediteranian ili kufika Ulaya kusaka maisha bora ambapo 3500 kati yao walipoteza maisha.