Simonovic aeleza matumaini yake baada ya ziara Sudan Kusini

9 Februari 2015

Baada ya ziara yake nchini Sudan Kusini, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Ivan Šimonović, amesema licha ya mapigano kupungua nchini humo, idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka hadi kufikia milioni 2.5, wengine 500,000 wakiwa wametafuta hifadhi katika nchi jirani.

Amesema amekutana na watu ambao wamefiwa familia yao yote na wasichana ambao wametumikishwa kingono na waasi.

Ivan Šimonović ameongeza kwamba, licha ya mapigano baina ya pande kinzani kwenye chama cha Sudan People's Liberation Movement, SPLM, kuna mapigano mengine baina ya makabila au koo tofauti katika kabila moja, huku uhalifu na ukatili wa kijinsia ukiendelea.

Hata hivyo, amesema matumaini yapo, akipongeza serikali kwa kuridhia baadhi ya mikataba ya kimataifa juu ya haki za binadamu.

Aidha, kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu uliofanyika nchini humo, ameeleza kwamba matokeo ya uchunguzi ulioendeshwa na Muungano wa Afrika yanatakiwa kutangazwa baada ya makubaliano ya amani kutimizwa.

Hatimaye ametoa wito kwa raia wote wa Sudan Kusini:

“ Ingawa ni Rais Kiir na Daktari Machar tu ambao wanahitajika ili kumaliza vita na kusaini makubaliano ya amani, wengine wengi zaidi wanahitajika ili kuhakikisha amani endelevu. Utaratibu wa amani unaoendelea, ili uwe endelevu, unapaswa kushirikisha wazee, viongozi wa kidini, vijana, wanawake, na wadau wengine wa jamii”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter