Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya magari ya misaada ni ukiukwaji wa sheria:

Mashambulizi dhidi ya magari ya misaada ni ukiukwaji wa sheria:

Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Adnan Khan amelaani vikali mashambulio ya Jumapili dhidi ya wafanyakazi wa shirika la hilal nyekundu nchini humo yaliyosababisha vifo vya wafanyakazi watatu wa kusambaza misaada.

Bwana Khan ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu nchin Sudan amesema wafanyakazi hao walikuwa sehemu ya timu iliyokuwa inafuatilia usambazaji wa misaada ya chakula inayotolewa na Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Kurmuk, jimbo la Blue Nile.

Katika taarifa yake ametuma rambirambi kwa familia na jamaa za waliouawa huku akiwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.

Ametoa wito kwa pande zote kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi wanaotoa misaada akisema kuwa mashambulio dhidi ya misafara ya magari  kunakwamisha usambazajiwa misaada na pia ni kinyume na sheria za kimataifa za usaidizi wa kibinadamu.

Tangu kuzuka kwa mzozo huko Kordofan Kusini na Blue Nile mwaka 2011, wasambazaji misaada wamekuwa wanakumbwa na mkwamo katika kupitisha misaada kwenye maeneo yanayodhibitiwa na kikundi kilichojihami cha SPLM-North.