Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini wanahitaji amani, utulivu na usalama: Amos

Sudan Kusini wanahitaji amani, utulivu na usalama: Amos

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu usaidizi wa kibinadamu Valerie Amos amehitimisha ziara yake ya kujionea hali halisi huko Sudan Kusini akirejelea wito wa jamii ya kimataifa wa kutaka pande husika kwenye mzozo huo kurejesha amani.

Akizungumza mjini Juba, Bi.Amos amesema inaumiza moyo kushuhudia watu wakikumbwa na machungu kwenye nchi ambayo ni tajiri siyo tu kwa vipaji vya wananchi wake bali pia rasilimali.

Mkuu huyo wa OCHA ametolea mfano alipotembea eneo la Ayod, jimbo la Jonglei akifuatana na mjumbe maalum wa UNESCO, Forest Whitaker ambako wamekuta watu wamechoka kuishi kwa woga na hofu bila huduma za msingi.

Amesema iwapo mapigano hayo yaliyoanza Disemba 2013 yataendelea, basi kizazi cha watoto wa Sudan Kusini kitatoweka, hali kadhalika maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii yatakwama.

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwezesha ombi la kifedha la dola Bilioni 1.8 ili kufikia watu zaidi ya Milioni Nne wenye uhitaji nchini Sudan Kusini.