Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shukrani Saudia kwa kujitoa kwa hali na mali: Ban

Shukrani Saudia kwa kujitoa kwa hali na mali: Ban

Umoja wa Mataifa umeisifu Saudi Arabia kwa jinsi inavyojitoa kwa hali na mali katika kusaidia majanga yanayokumba ukanda huo. Ni kauli ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyoitoa wakati alipokutana na waandishi wa habari mjini Riyadhi, baada ya mazungumzo yake na Mfalme Salman bin Abdulaziz wa nchi hiyo.

Ban ambaye yuko Saudia kuhani msiba  amesema kujitoa huko ni pamoja na harakati za hayati mfalme Abdullah Bin Abdulaziz Al-Saud za kusaidia kuondokana na njaa duniani na hata kujenga uhusiano mwema baina ya watu wenye imani mbali mbali za dini.

Amesema alisaidia kufanikisha maendeleo Saudi Arabia kwa kuweka mwongozo wa kipekee wa ustawi, sambamba na kushughulikia changamoto za kikanda na kimataifa ikiwemo harakati dhidi ya ugaidi wakati wa ghasia na mabadiliko.

Halikadhalika Ban na Mfalme Salman wamejadili Yemen, Iraq halikadhalika Syria ambapo amelaani vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na pande zote nchini Syria akisema suluhu la mzozo huo ni la kisiasa pekee na si vinginevyo.

 Kuhusu haki za binadamu Katibu Mkuu amesema..

(Sauti ya Ban)

“Naisihi serikali ya Saudi Arabia iendeleze ushirikiano wake wa dhati na Umoja wa Mataifa ili tuweze kushinda changamoto nyingi zinazokumba eneo hili na dunia yetu. Maendeleo yanatutaka tulinde haki za binadamu, ikiwemo haki za wanawake, na kuheshimu haki zote za msingi.”