Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wakimbizi wa ndani Ukraine yakabiria Milioni

Idadi ya wakimbizi wa ndani Ukraine yakabiria Milioni

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeripoti kuwa mapigano huko Mashariki ya Ukraine kwenye eneo la Donetsk yamesabaisha watu wengi zaidi kukimbia makwao na kwa hivyo kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia karibu watu milioni moja.Wizara ya Sera ya Jamii ya Ukraine imesema idadi ya wakimbizi wa ndani kote nchini ni 980,000, ikisema dadi hiyo inatarajiwa kuongezeka wakati ambapo watu wengine zaidi wanaofurushwa kutoka makwao watakaposajiliwa.

Msemaji wa UNHCR, Adrian Edwards amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa timu ya UNHCR imeripoti mapigano makali huko Donetsk katika kipindi cha wiki mbili zilizopita , mapigano ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu na kudorora kwa huduma za msingi.

Kuhusu msaada kwa waathiriwa hao, Bwana Edwards amesema serikali za mitaa zimeanza kuokoa watu kutoka maeneo ya vita, lakini wengi bado wamejikuta katikati ya mapigano, ikiwa ni pamoja na kujificha katika mahandaki yaliyo chini ya nyumba na hata majengo ambayo yanashambuliwa mara kwa mara.