Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tatizo la chakula lazidi Sudan Kusini:FAO

Tatizo la chakula lazidi Sudan Kusini:FAO

Shirika la Chakula na Kilimo FAO limeonya ijumaa hii kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama wa chakula nchini Sudan Kusini, huku watu milioni 2.5, sawa na asilimia 20 ya raia wote nchini humo wakiathirika na njaa wakati mapigano yanapoendelea. Mwaka uliopita wakati ghasia ilipoibuka, idadi hiyo ilikuwa ni watu milioni moja tu.

Sababu kubwa ya hali hii ya njaa ni mapigano ambayo yamezuia watu kuendelea na shughuli zao za ukulima. Kwa mujibu wa FAO, asilimia 40 tu ya ardhi inayolimwa kawaida imelimwa mwaka huu. Aidha shirika hilo limesema mikoa mingine ya Sudan Kusini ina uwezo wa kuzalisha mazao ya kutosha kwa raia wote lakini ukosefu wa miundombinu, vifaa na teknolojia unazuia upatikanaji wa mazao mengi zaidi.

Serge Tissot ni Kaimu Mwakilishi wa FAO Sudan Kusini. Anaeleza kwamba njaa inaathiri maeneo ambapo jamii imepokea wakimbizi wa ndani.

"Kwa hiyo jamii inapaswa kulisha watu wengi zaidi kuliko kawaida. Kawaida, kwenye mwaka wa kawaida, tayari kuna pengo, mwisho wa kiangazi, wakati wa kusubiri mavuno mengine. Pengo hilo la mwambo ni katika Machi na Mei, na mwaka huu, mwambo utaathiri watu wengi "

Shirika la FAO limetoa wito kwa ufadhili ili kuwapatia jamii hizo vifaa vya kilimo hasa mbegu za kupanda.