Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMF yakwamua ulipaji madeni kwa nchi zilizokumbwa na Ebola

IMF yakwamua ulipaji madeni kwa nchi zilizokumbwa na Ebola

Shirika la fedha duniani IMF limetoa jumla ya dola Milioni 100 kwa nchi tatu za Afrika Magharibi zilizoathiriwa zaidi na Ebola ili kusaidia ulipaji wa madeni yake.

Sean Nolan, Naibu Mkurugenzi wa mkakati na sera IMF amesema nchi hizo ni Guinea, Liberia na Sierra Leone na lengo ni kupunguza athari za mzigo wa ulipaji madeni wakati huu ambapo nchi hizo zinahaha kukabiliana na mlipuko wa Ebola.

Amesema fedha hizo ni nyongeza ya dola Milioni 130 zilizotolewa chini ya mpango wa dharura wa IFM mwezi Septemba sambamba na dola Milioni 160 zilizoidhinshwa kama mkopo mwezi huu.

Nolan amesema fedha hizo zinatoka kwenye mfuko mpya maalum wa usaidizi CCR na utakuwa unatumika kuweka unafuu wa madeni kwa nchi za vipato vya chini zilizokumbwa na majanga ya asili yanayoweza kuleta madhara nje ya mipaka yao.