Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi : UM na wasiwasi kwa kushikiliwa kwa mwandishi Rugurika

Burundi : UM na wasiwasi kwa kushikiliwa kwa mwandishi Rugurika

Ofisi ya Haki za Binadamu imeelezea wasiwasi wake kuhusu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa mwandishi wa habari Bob Rugurika nchini Burundi, ikisema kitendo hicho kinadhalilisha uhuru wa kujieleza nchini humo.

Rugurika ambaye ni mkurugenzi wa redio huru ya kijamii nchini humo, Radio Publique Africaine, ameshikiliwa korokoroni tangu tarehe 28 Januari , baada ya redio yake kudaiwa kutoa shutuma kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika la upelelezi nchini humo wameshirikiana katika mauaji ya watawa watati wa kike wa Italia, yaliyotokea Septemba, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Ravina Shamdasani, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, mwandishi huyu yuko hatarini kufungwa kwa muda mrefu, mahakama ya Burundi ikiwa imemshtaki kwa kushiriki katika mauaji hayo. Jumatano hii, mahakama imekataa kumwachilia huru wakati akisubiri kesi yake.

(Sauti ya Ravina)

« Kesi ya Rugurika inatia wasiwasi sana juu ya uhuru wa kujieleza nchini Burundi, hasa wakati wa maandalizi ya uchaguzi. Tunatoa wito kwa mamlaka za serikali izihakikishe kwamba kesi ya Rugurika izingatie viwango vya kimataifa, ili atendewe haki. Hakuna mtu anayepaswa kushtakiwa akiwa anatekeleza haki yake ya msingi ya kujieleza huru »