Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza lalaani vikali mashambulizi ya Boko Haram

Baraza lalaani vikali mashambulizi ya Boko Haram

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mwendelezo wa mashambulio yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram dhidi ya raia na askari.

Miongoni mwa mashambulio hayo niyale ya tarehe Tatu na Nne Februari kwenye mpaka kati ya Nigeria na Cameroon ambako askari wa 26 na raia waliuawa na wengine walijeruhiwa.

23 kati ya waliouawa ni askari wa Chad ilihali watatu ni wa Cameroon.

Wajumbe hao wamesema mashambulio yaliyofanywa na askari wa Chad dhidi ya Boko Haram kwenye ardhi ya Nigeria yalitekelezwa kwa makubaliano na serikali ya Nigeria ambyo mamlaka yake inaheshimiwa.

Baraza limetuma rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali za Chad na Cameroon na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa mashambulio hayo ya kikatili.

Halikadhalika wamesifu kasi ya usaidizi iliyochukuliwa na jeshi la Chad dhidi ya mashambulio ya Boko Haram nchini Nigeria kulikosababisha kutwaliwa kwa eneo lililokuwa linashikiliwa na kikundi hicho sambamba na vifaa na silaha.