Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukanda uungane kutokomeza FDLR: Djinnit

Ukanda uungane kutokomeza FDLR: Djinnit

Mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa maziwa makuu Said Djinnit ametaka nchi za ukanda huo kuungana ili kutokomeza kikundi cha waasi cha FDLR huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Bwana Djinnit amesema hayo mwishoni mwa ziara yake nchini Rwanda ambako amekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Louise Mushikiwabo.

Kwa mantiki hiyo ameelezea azma yake ya kuendelea kuishawishi serikali ya DRC inayoungwa mkono na ujumbe wa Umoja wa Mataifa MONUSCO ili kuhakikisha operesheni ya kijeshi inayoendelea dhidi ya FDLR inakuwa thabiti lakini isilete machungu kwa raia wasio na hatia.

Halikadhalika ameiomba Rwanda iendeleaa kushiriki kwenye mkataba wa amani, usalama na ushirikiano kwenye ukanda wa maziwa makuu uliotiwa saini huko Addis Abba Ethiopia mwezi Februari mwaka 2013.

Bwana Djinnit pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Rwanda kwa ushirikiano wake na DRC katika kuwarejesha makwao waliokuwa wapiganaji wa kikundi cha M23.