Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sehemu za utamaduni ni fursa mpya ya utalii endelevu

Sehemu za utamaduni ni fursa mpya ya utalii endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na lile la utalii duniani, UNWTO, yameshirikiana kuleta pamoja mawaziri wa utalii na utamaduni kutoka duniani kote ili kujadili kuhusu uhusiano baina ya utamaduni na utalii, katika kongamano la kimataifa linalofanyika Siem Reap, nchini Cambodia, kuanzia Jumatano hii hadi tarehe 6 Februari.

Utalii unaolenga sehemu za utamaduni ni fursa mpya kwa ukuaji wa uchumi, kijamii na utunzaji wa utamaduni, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNESCO na UNWTO. Kongamano la kwanza la utalii na utamaduni linalofanyika nchini Cambodia litawezesha wataalam na watungaji sera kubaini fursa hizo na changamoto zinazokumba maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo kwa njia ya ujumbe wa video, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova, amesema UNESCO inajitahidi kuongeza uhusiano baina ya utamaduni na utalii, hapo akisema:

“ Utamaduni ni sisi, unatuwezesha kujitambua, ni njia ya kuimarisha heshima na uelewano baina ya watu. Pia ni njia ya kutengenza mamilioni ya nafasi za ajira, na kuimarisha maisha ya watu. Ndio maana kutunza urithi wa utamaduni kunapaswa kwenda sambamba na utalii endelevu. Naona ni ujumbe wa msingi wa kongamano hili la utamaduni na utalii”