Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP na IRI kuimarisha ushirikiano kuhusu utawala bora duniani

UNDP na IRI kuimarisha ushirikiano kuhusu utawala bora duniani

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na taasisi ya kimataifa ya IRI wametiliana saini makubaliano  ya maelewano yenye lengo la kuimarisha majukumu yao kuhusu utawala bora na siasa shirikishi za vyama vingi kote duniani.

Mtawala mkuu msaidizi wa UNDP Magdy Martínez-Solimán amesema katika taarifa kuwa taasisi hizo mbili zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu kwani zina mambo mengi yanayofanana na hivyo makubaliano hayo yataimarisha juhudi zao za kusaidia mataifa kwenye masuala kadhaa ikiwemo usuluhishi wa amani wa mizozo na utawala bora.

Kupitia makubaliano hayo UNDP na IRI watabadilishana utaalamu na uelewa kuhusu masuala ya ujumuishi, utawala bora na ushiriki wa raia kwenye michakato ya uchaguzi.

Halikadhalika watashirikiana kwenye kuibua mbinu bunifu za kuhakikisha misaada wanayotoa inaleta mabadiliko chanya kwa walengwa.

Naye Mkuu wa IRI au International Republican Institute, Balozi Mark Green amesema ushirika huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za sasa za demokrasia.