Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yasikitishwa na habari za kuteketezwa vitabu Mosul

UNESCO yasikitishwa na habari za kuteketezwa vitabu Mosul

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO Irina Bokova, ameelezea kusikitishwa na ripoti za uharibifu wa idadi kubwa ya vitabu kwenye majengo ya kumbukumbu, maktaba na vyuo vikuu huko Mosul, Iraq.

Bi Bokova amesema kuteketezwa kwa vitabu kunawakilisha awamu mpya ya uharibifu wa utamaduni  unaotendwa katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya msimamo mkali yaliyojihami nchini Iraq. Ameongeza kuwa uharibifu huo ni sehemu ya ukatili dhidi ya makundi ya walio wachache, unaolenga kuangamiza utofauti wa kitamaduni ambao ni sehemu muhimu ya watu wa Iraq.

Kwa mujibu wa ripoti kadhaa za vyombo vya habari, maelfu ya vitabu kuhusu falsafa, sheria, sayansi na ushairi vimeteketezwa kwa kukusudia katika kipindi cha wiki chache zilizopita. Kikithibitishwa, Bi Bokova amesema kitendo hicho kitakuwa moja ya vitendo vya uharibifu mbaya zaidi kwa vitabu maktabani katika historia ya mwanadamu.

Akikumbusha kuhusu kutekezwa kwa nakala za kumbukumbu kwenye kituo cha Ahmed Baba, mjini Timbuktu, Mali, Bi Bokova amesema kuteketeza vitabu ni shambulizi dhidi ya utamaduni, maarifa na kumbukumbu.