Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Sudan Kusini afikianeni mapema kuhusu utawala: Ban

Viongozi wa Sudan Kusini afikianeni mapema kuhusu utawala: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametambua matokeo ya awamu ay mwisho ya mashauriano kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu rais wake wa zamani Dkt. Riek Machar kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini tarehe Pili mwezi huu mjini Addis Ababa.

Hata hivyo Ban amesema anasikitishwa kuwa hakuna upande wowote ambao umelegeza masharti ya kuwa na makubaliano ya pamoja kuhusu utaratibu wa kuanzisha serikali ya pamoja.

Ban amenukuliwa na msemaji wake akisisitiza kuwa hakuna amani endelevu inaweza kupatiakana Sudan Kusini bila viongozi wa nchi hiyo kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya maslahi yao binafsi.

Kwa mantiki hiyo amesisitiza udharura wa mkataba shirikishi wa amani unaoshughulikia masuala ya msingi ya marekebisho ya kitaasisi, utawala wa kiuchumi, maridhiano na uwajibikaji kwa vitendo vya uhalifu vilivyotekelezwa tangu kuibuka kwa mzozo nchini Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013.

Amerejelea wito wake wa kutaka pande kinzani kuzingatia mkataba wa kumaliza chuki uliotiwa saini tarehe 23 mwezi Januari mwaka 2014 huku akitaka wajiandae kwa awamu ijayo ya mazungumzo.

Halikadhalika ameshukuru IGAD kwa jitihada zake za kuleta maridhiano Sudan Kusini na kuhakikisha utayari wa Umoja wa Mataifa na wadau wake kusaidia ili kuleta pamoja makundi yanayokinzana nchini humo.