Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtambo wa kwanza wa kutengeneza silaha za kemikali Syria waharibiwa

Mtambo wa kwanza wa kutengeneza silaha za kemikali Syria waharibiwa

Shirika la Kupinga Silaha za Kemikali, OPCW, limetangaza kuwa mtambo wa kwanza uliotumiwa zamani kutengeneza silaha za kemikali nchini Syria umeharibiwa katika shughuli iliyokamilika mnamo Januari 31, 2015.

Wakaguzi wa OPCW walihakiki na kutangaza kuharibiwa kwa mtambo huo, ambao ulikuwa wa kwanza miongoni mwa mitambo 12 kama hiyo iliyopangwa kuharibiwa.

Taarifa iliyotolewa na OPCW imesema kuwa kazi na maandalizi ya kuiharibu mitambo 11 iliyosalia yanaendelea. Mkurugenzi Mkuu wa OPCW, Ahmet Üzümcü amekaribisha kuharibiwa kwa mtambo huo, ambako amesema kulicheleweshwa kwa sababu za kitaaluma, na kuongeza kuwa anatarajia kuwa kazi ya kuharibu mitambo iliyosalia itaendelea kama ilivyopangwa.

OPCW imethibitisha kuwa asilimia 98 ya silaha za kemikali zilizowekwa bayana na serikali ya Syria zimeteketezwa.