Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendesha Mashtaka wa ICC azungumzia uchaguzi Nigeria

Mwendesha Mashtaka wa ICC azungumzia uchaguzi Nigeria

Huku Nigeria ikielekea uchaguzi mkuu kuanzia tarehe 14 mwezi huu, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, Fatou Bensouda amewasihi wanasiasa, vyama vya kisiasa na wafuasi wao kuimarisha dhamira yao ya kuepukana na ghasia wakati wa uchaguzi huu kwa muktadha ya ahadi wagombea wa urais walitoa hivi majuzi. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Bi Bensouda katika taarifa amewakumbusha viongozi hao kwamba wakati ambapo ghasia zimetanda katika baadhi ya maeneo ya nchi, ICC ina mamlaka ya kuanzisha kesi ya makosa yaliyotendwa nchini Nigeria au na raia wa Nigeria kuanzia Julai Mosi mwaka 2002 kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.

Amesema uzoefu umeonyesha kwamba ushindani wa kisiasa unaweza kuchochea kulipuka kwa vurugu au uhalifu dhidi ya umma ambavyo vinaweza kushtua mwanadamu.

Halikadhalika, Bensouda amesema mtu yeyote ambaye anachochea au kutekeleza vitendo vya vurugu ikiwa ni pamoja na kuagiza, kuomba, na kuwahamasisha au kusababisha kwa namna yoyote utekelezaji wa uhalifu chini ya Mamlaka ya ICC atashtakiwa kwenye mahakama ya Nigeria au ICC.