Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya Boko Haram

Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya Boko Haram

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limelaani vikali kuongezeka kwa mashambulizi kunakotekelezwa na kundi la Boko Haram, likiwemo lile lililofanywa mnamo Februari mosi Maiduguri, jimbo la Borno, Nigeria, pamoja na mashambulizi yanayoongezeka kwenye ukanda wa ziwa Chad.

Wamelaani pia vikali mashambulizi dhidi ya vikosi vya Chad vilivyopelekwa kusaidia kupigana na kundi hilo nchini Cameroon mnamo Januari 29 na 30, ambayo yalisababisha vifo vya wanajeshi 4 wa Chad na kuwajeruhi 12 wengine.

Wanachama wa Baraza la Usalama wamepeleka rambi rambi zao kwa familia za wahanga na kuwapa pole waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kikatili, na kwa serikali za Nigeria na Chad.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama pia wamekariri kusikitishwa kwao kwamba vitendo vya Boko Haram vinadhoofisha amani na usalama kwenye ukanda wa Afrika Magharibi na Kati. Wametoa wito kwa ukanda huo kuimarisha operesheni za kikanda za kijeshi ili kukabiliana na Boko Haram ipasavyo.