Wafanyakazi wa ndege wa WFP walioshikiliwa na SPLM-N wamerejea salama

2 Februari 2015

Raia sita wa Bulgaria waliokuwa wameshikiliwa na kundi la waasi la Sudan People’s Liberation Army- North, SPLM-N katika mkoa wa Kordofan Kusini nchini Sudan, wameachiwa huru na kukabidhiwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula, WFP wakiwa salama. Taarifa Kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa Ya Grace)

Watu hao sita walishikiliwa mateka pale ndege yao aina ya helikopta iliyokodishwa na WFP ilipolazimishwa kutua katika mkoa wa Kordofan na kundi la waasi la Sudan People’s Liberation Army- North, SPLM-N wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa WFP, wafanyikazi hao waliwasili katika ofisi ya WFP ilioko Yida, mpakani Kordofan Kusini leo asubuhi.  Kuachiliwa kwa wafanyakazi hao kunafuatia juhudi za shirika la wanawake la the New Sudan Women’s League ambalo lilishauriana na kundi la SPLM-N.

Halikadhalika, WFP pia ilishirikiana na serikali za Sudan na Sudan Kusini katika kutambua na kuwaokoa wafanyakazi hao punde tu mawasiliano na helikopta yalipopotea.

Kwa muktadha huo,  WFP imeshukuru serikali ya Sudan hasa kwa msaada wake katika kuhakikisha wafanyakazi hao wamerudi salama.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter