Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati umetimia wa kumaliza kabisa tishio la FDLR DRC- Ban

Wakati umetimia wa kumaliza kabisa tishio la FDLR DRC- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa licha ya juhudi zilizofanywa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC likisaidiwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MONUSCO katika kumaliza vitendo vya makundi yenye silaha na kuwalinda wananchi,  makumi ya watu bado wameuawa katika miezi michache iliyopita kwenye eneo la Beni.

Akizungumza kwenye mkutano wa tano wa kutathmini mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kuhusu DRC na ukanda wa Maziwa Makuu, Addisa Ababa, Bwana Ban amesema janga hilo la mauaji linaweka msisitizo umuhimu wa kuyatokomeza makundi yote haramu yaliyojihami kwenye eneo hilo.

Kwa Mantiki hiyo, Katibu Mkuu amekaribisha msimamo wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya FDLR, na kuelezea kufurahia tangazo la serikali ya DRC kuanza operesheni za kijeshi hivi karibuni, ikisaidiwa na MONUSCO.

Ban amesema kuwa Umoja wa Mataifa u tayari kusaidia mamlaka za DRC na jeshi lake katika kufikia lengo la kuondoa tishio la FDLR, huku akielezea pia kusikitishwa na mwendo wa pole wa utekelezaji wa makubaliano ya Nairobi, ambayo pamoja na mambo mengine, yalitoa mwelekeo kuhusu mchakato wa msamaha kwa baadhi ya waasi wa zamani wa M23.

Ametoa wito kwa serikali za DRC, Rwanda na Uganda kuongeza kasi ya juhudi za kuutekeleza mchakato huo haraka iwezekanavyo.