Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na Waziri Diop wa Mali

Ban akutana na Waziri Diop wa Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, pembezoni mwa mkutano mkuu wa kila mwaka wa Muungano wa Afrika, AU, mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Ban amelaani matukio ya hivi karibuni Gao, kaskazini mwa Mali, huku akikariri ahadi ya Umoja wa Mataifa kufanya kazi pamoja na serikali ya Mali ili kupata habari kamili kuhusu matukio hayo.

Ban ameitia moyo serikali ya Mali iendelee kuonyesha uongozi wake na kushiriki kwenye mchakato wa amani kwa njia inayojenga, kabla ya awamu ijayo ya mazungumzo ya amani kuhusu Mali mjini Algiers, mwezi Februari. Wamekubaliana kuhusu haja ya serikali ya Mali kuongeza juhudi za kushughulikia changamoto zilizopo kwenye mchakato huo wa amani, huku waziri Diop akikariri uungaji mkono wa serikali yake kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Mali, MINUSMA.

Ban ameipongeza tena serikali ya Mali kuhusu jinsi ilivyodhibiti mlipuko wa Ebola, na kuihimiza iendelee kuimarisha juhudi za kuzuia mlipuko tena.