Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano katika kupambana na Ebola ni mfano wa kuendelezwa- Ban

Mshikamano katika kupambana na Ebola ni mfano wa kuendelezwa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa mlipuko wa Ebola umekuwa moja ya changamoto sugu zaidi iliyolikumba bara Afrika mwaka mmoja uliopita, lakini akaongeza kuwa amejivunia kazi iliyofanywa kwa ushirikiano katika kupambana na mlipuko huo.

Bwana Ban ameyasema hayo wakati akikutana na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, ambako mkutano mkuu wa kila mwaka wa Muungano wa Afrika, AU unafanyika, akitaja kuwa AU imekuwa mstari wa mbele katika dhidi ya Ebola.

Ban amesifu mshikamano uliodhihirishwa katika vita dhidi ya Ebola, akitaja michango ya nchi wanachama wa AU katika kutoa rasilmali, utaalam na vifaa tiba, huku mamia ya wahudumu wa afya wakipelekwa kwenye nchi zilizoathiriwa. Katibu Mkuu amesema mshikamano huo unapaswa kuendelezwa hadi pale Ebola itakapotokomezwa katika kila nchi, na hata wakati wa nchi hizo kujikwamua.

Mwanzoni mwa mkutano huo na waandishi wa habari, Ban amelaani vikali shambulio la bomu kaskazini mwa Sinai, Misri mapema wiki hii, likiwaua watu kadhaa na kuwajeruhi wengine wengi.